Alhamisi 22 Oktoba 2026 - 14:00
Ongezeko la Maandamano Katika Bara la Ulaya na Mdororo wa Kimaadili wa Ustaarabu wa Magharibi

Hawza/ Kinachoshuhudiwa leo katika mitaa ya Ufaransa na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya dhidi ya wananchi wanaoandamana ni, kwa hakika, utekelezaji wa kidikteta uliojificha chini ya mwavuli wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia kuongezeka maandamano ya wananchi katika baadhi ya nchi za Ulaya, hususan Ufaransa. Kama wanavyobainisha wanafikra mbalimbali, maandamano yamezuka katika moyo wa Ulaya, bara ambalo kwa miongo mingi limejiona kuwa dira ya “utawala wenye mantiki”, na katika maeneo mengi maandamano hayo yamegeuka kuwa ghasia. Hili ndilo bara ambalo kwa miaka mingi limekuwa likidai kwamba ustaarabu wa Magharibi na Ulaya ni hatua ya mwisho katika historia ya maendeleo ya mwanadamu, na kwamba baada yake hakuna tena chaguo wala mbadala mwingine wa ukuaji na maendeleo ya binadamu.

Maandamano nchini Ufaransa, Italia, Ubelgiji na Ureno, licha ya kutofautiana kwa mazingira na madai yanayoyachochea, yamejikita katika mkusanyiko wa matatizo yanayowagusa wananchi moja kwa moja. Miongoni mwa matatizo hayo ni ongezeko lisilo la kawaida la gharama za maisha, kupungua kwa fursa za kupata makazi, changamoto za kulipa mishahara, kushuka kiwango cha ubora wa huduma za umma, pamoja na kuendelea kupanda gharama za elimu.

Ulaya Inayojinasibu kwa Ustaarabu na Taswira ya Udanganyifu ya Maendeleo

Hasa nchini Ufaransa, inaweza kusemwa kuwa maandamano makubwa yamehusishwa na kutoridhika wananchi kuhusu hali ya huduma za umma na gharama za maisha. Nchini Ubelgiji, wanafunzi wameandamana kupinga ongezeko la gharama na kupungua fursa za kupata elimu ya juu. Nchini Ureno, mgogoro wa makazi na shinikizo la gharama za kila siku vimekuwa miongoni mwa sababu kuu za mikusanyiko ya waandamanaji.

Maandamano Dhidi ya Ukosefu wa Haki Katika Moyo wa Ulaya

Kwa mujibu wa Rasoul Lotfi, mwandishi wa habari na mwanaharakati wa vyombo vya habari, kutokea kwa maandamano haya kwa wakati mmoja kunatoa fursa ya kuibua suala la pamoja, nalo ni uhusiano kati ya ahadi za maendeleo na uwezekano halisi wa kuishi katika jamii inayodaiwa kuwa imeendelea.

Amesisitiza pia kwamba taswira inayotawala kuhusu “mfumo wa Ulaya” ni mchanganyiko unaovutia wa soko huria, demokrasia ya bunge, usawa katika elimu na mfumo mpana wa ustawi wa jamii. Hata hivyo, kuchunguza chimbuko na historia ya mfumo huo kunafichua uhalisia tofauti.

Amebainisha kuwa jambo la kuzingatia ni kwamba maeneo hasa ambako maandamano haya yameanzia ni “shule” na “nyumba”. Maeneo haya mawili ni mihimili muhimu ya kipekee ya “uzalishaji upya wa kijamii” na njia zinazounganisha kizazi kimoja na kingine.

Kupitia shule, ustaarabu humuahidi mwanadamu mpya kwamba akilikubali mfumo wa alama na kanuni za kijamii zilizowekwa na kuongeza uwezo wake, basi mustakabali wake utakuwa salama. Kwa upande mwingine, kupitia nyumba mfumo huo humuhakikishia kwamba katika ulimwengu wa kimwili atakuwa na sehemu salama na yenye utulivu ambayo ni yake.

Lotfi ameongeza kuwa ni jambo la kawaida kutarajia hali kuwa ngumu na tata pale mfumo tawala unaposhindwa kutekeleza ahadi hizi mbili muhimu na kushindwa kutoa jibu kwa ukiukaji wake ulio wazi.

Katika mazingira hayo, shule huacha kuwa ngazi ya kupanda kutoka tabaka moja la kijamii kwenda jingine, huku nyumba nayo ikigeuka kuwa makazi yasiyofikika kwa wananchi wengi.

Kwa hiyo, mfumo tawala unapojibu madai ya kuboresha shule zilizochakaa na kutatua mgogoro wa makazi kwa kuongeza udhibiti wa kiusalama na ukandamizaji, na badala ya “kufanya upya mkataba wa kijamii” ukaamua “kusimamia matokeo kwa kutumia polisi na vyombo vya usalama”, pazia la madai ya utawala wenye mantiki huanguka. Kuanzia hapo, tunashuhudia kudhoofika kwa mfumo wa Ulaya.

Dhoruba ya Hasira za Wananchi Dhidi ya Wanasiasa wa Bara la Ulaya

Ukweli ni kwamba dhoruba ya hasira za wananchi dhidi ya mazingira magumu na yasiyofaa ya maisha, kuanzia Ufaransa hadi nchi nyingine za Ulaya Magharibi na Ulaya ya Kati, ni jambo lisiloweza kukanushwa.

Hali hii inajiri wakati vyombo vya habari vikiripoti kuendelea kwa maandamano makubwa na yenye vurugu katika maeneo mbalimbali ya Ulaya, yakipinga sera za kubana matumizi ya serikali na hali mbaya ya kiuchumi. Inaonekana kuwa maandamano dhidi ya wanasiasa wa bara la Ulaya yanaweza kuendelea kushika kasi zaidi.

Jambo ambalo vyombo vya habari vinavyohusishwa na mfumo wa utawala wa kibeberu haviwezi kulificha ni kwamba, pembezoni mwa maandamano katika maeneo mengi, kumetokea mapigano makali. Kwa mfano, jijini Milan, Italia, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi, katika baadhi ya miji, hasa, magari ya kunyunyizia maji kwa shinikizo kubwa yalitumika dhidi ya waandamanaji.

Vilevile, mapigano makali yalitokea katika miji ya Brussels na Liège nchini Ubelgiji, pamoja na Tirana na miji mingine ya Albania. Kutokana na matukio hayo, mamia ya watu wamekamatwa katika maandamano hayo. Hata hivyo, hali nchini Ufaransa imeripotiwa kuwa mbaya zaidi ikilinganishwa na nchi nyingine.

Maandamano Yamevuka Mipaka ya Wanafunzi wa Shule Nchini Ufaransa

Maandamano nchini Ufaransa yameingia katika wiki yake ya nne, huku serikali ikiwa bado haijachukua hatua madhubuti za kushughulikia madai ya waandamanaji. Kwa sababu hiyo, waandamanaji wameelekeza hasira zao dhidi ya mali za serikali.

Katika siku hizi zenye mvutano mkubwa, serikali ya Ufaransa inajaribu kudhibiti wigo wa maandamano kwa kuweka vikwazo mbalimbali. Hata hivyo, kutoridhika huku hakuwahusu tena wanafunzi wa shule pekee, bali kumeenea katika sekta nyingine za jamii na kugeuka kuwa harakati pana zaidi.

Katika muktadha huo, wawakilishi wa vuguvugu la Gilets Jaunes (Wenye Fulana za Njano), ambao walifanya maandamano kwa miezi kadhaa katika kipindi cha kwanza cha urais wa Emmanuel Macron, wametoa wito wa kuandaliwa duru mpya ya maandamano.

Waandamanaji hao wa Gilets Jaunes, ambao wamekasirishwa na ongezeko la gharama za maisha, waliungana mwishoni mwa wiki iliyopita na wanafunzi ambao katika wiki za hivi karibuni walikuwa wamefanya mikusanyiko na kufunga shule kupinga uhaba wa walimu na hali mbaya ya shule.

Kashfa ya Viongozi Yafichuka Baada ya Kuongezeka kwa Maandamano

Kwa miongo kadhaa, serikali ya Ufaransa imekuwa ikijitahidi kujionyesha kama serikali inayotetea uhuru. Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, sifa yake imeendelea kuchafuliwa, na ulimwengu umeanza kutambua kiwango cha ukali wa serikali hiyo na namna inavyotumia nguvu kubwa kukabiliana na kila maandamano.

Kuanzia tukio la vuguvugu la Gilets Jaunes mwaka 2019 hadi harakati za sasa za wanafunzi wa vyuo na shule, Ikulu ya Élysée imekuwa ikikandamiza kila sauti ya upinzani kwa ukali mkubwa.

Paris, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikijitangaza kuwa kitovu cha demokrasia na uhuru wa kujieleza, sasa, inapokabiliwa hata na ukosoaji wa ndani, imeonyesha sura yake ya kimabavu. Hali hii imeibua taswira kwamba demokrasia ya Ufaransa inaheshimiwa tu pale inapohudumia maslahi ya wakazi wa Ikulu ya Élysée.

Kinachoshuhudiwa leo katika mitaa ya Ufaransa dhidi ya wanafunzi wa shule na vyuo wanaoandamana ni utekelezaji wa kidikteta uliojificha chini ya mwavuli wa haki za binadamu.

Inaonekana kwamba, kwa mtazamo wa Paris, uhuru wa kujieleza unamaanisha tu kuwa na haki ya kuyatukana mambo matakatifu, badala ya kuwa na haki ya kupinga sera dhalimu za utawala.

Vijana wa Ufaransa Wanadai Haki Zao za Msingi na za Kawaida Tu

Hali hii inajiri wakati kizazi kipya cha Ufaransa, wakiwemo wanafunzi wa shule na vyuo wanaoandamana, hakidai chochote zaidi ya haki zake za msingi na za kawaida. Kwa mfano, hivi karibuni mmoja wa wanafunzi wa Kifaransa aliyeshiriki maandamano alisema katika mahojiano na chombo kimoja cha habari: “Tunataka tu kuwa na mwalimu na vitabu ili tuweze kupata diploma. Tumekaa miezi sita bila mwalimu, haiwezekani wanafunzi 35 kukaa katika darasa moja wakati wa joto la kiangazi.”

Haya ni madai ya msingi kabisa ambayo hata katika nchi maskini zaidi, yanaweza kushughulikiwa kwa njia za kiraia. Hata hivyo, jibu la serikali ya Ufaransa kwa madai haya rahisi na ya msingi limekuwa ukandamizaji, matumizi ya nguvu kubwa na hatua za kipolisi.

Mdororo wa Kimaadili wa Wanaojinasibu Kutetea Haki za Binadamu

Mabadiliko makubwa ya msimamo wa serikali ya Ufaransa katika kukabiliana na maandamano ni funzo kwa wale wanaozichukulia nchi za Magharibi kuwa mfano wa uhuru usio na mipaka.

Ufaransa, ambayo huingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine kwa kisingizio cha kuwatetea waandamanaji, inapokabiliwa na sauti za wananchi wake yenyewe, hukimbilia kutumia nguvu. Tofauti ya msingi katika namna Ikulu ya Élysée inavyoyaangalia maandamano ni ushahidi ulio wazi wa mdororo wa kimaadili wa mfumo wa kisiasa wa Ufaransa.

Katika mfumo huo, machafuko na mauaji ya polisi katika nchi huru huitwa harakati za kiraia, lakini maandamano tu yanapofanyika ndani ya ardhi ya Ufaransa, hutafsiriwa kuwa ni kuvuruga usalama wa taifa na kujibiwa kwa marungu na mabomu ya kutoa machozi.

Ripoti: Sayyid Muhammad Mahdi Mousavi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha